Kamati Maadili ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) imemfungia maisha Makamu wa Rais wa shirikisho hilo, Michael Wambura kutojihusisha na masuala ya soka kwa makosa matatu.
Taarifa ya TFF leo imesema kwamba hatua hiyo imechukuliwa kwa mujibu wa kifungu cha 73(1) (c) cha Kanuni za Maadili ya TFF Toleo la 2013.
Maamuzi hayo yamechukuliwa baada ya kikao cha kamati hiyo kilichoketi jana ambapo pamoja na mambo mengine, kilimjadili Wambura aliyefikishwa kwenye kamati hiyo kwa makosa matatu ya kupokea fedha za TFF malipo yasiyo halali, kugushi  barua na kushusha hadhi ya TFF.
Wambura alifikishwa kwenye kamati ya Maadili na Sekretarieti ya TFF baada ya Kamati ya Ukaguzi kukutana na kupitia mambo mbalimbali ya ukaguzi na suala hilo la Wambura kuonekana linatakiwa kufika kwenye Kamati ya Maadili.