Serikali Yatangaza Ajira Mpya, Yaelekeza namna ya kutuma maombi.
Serikali ya Tanzania kupitia Wakala wa Huduma za Ajira Tanzania (TaESA) imetangaza nafasi za kazi 10,000 kwa wananchi wote waliopo nchini kwenye mradi wa bomba la kusafirisha mafuta ghafi kutokea Hoima nchini Uganda hadi Chongoleani, Tanga.
Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Huduma za Ajira Tanzania (TaESA), Boniface Chandaruba
Hayo yamebainisha na Kaimu Mtendaji Mkuu wa TaESA, Boniface Chandaruba wakati alipokuwa anazungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam na kuwataka watanzania kujitokeza kujisajili ambapo zoezi hilo limeshaanza kuanzia sasa na litasitishwa Machi 30, 2018 ili waweze kuwatambua rasmi.
"Huu ni moja ya miradi mikubwa kutekelezwa hapa nchini ambao unategemea kugharimu Dola za Kimarekani 3.5 Billioni sawa na shillingi Trillion 8 za Kitanzania. Tanzania inayofursa kubwa ya ajira katika mradi huu wa ujenzi wa bomba la mafuta hivyo sisi kama TaESA tumepewa jukumu la kuwahamasisha watanzania waweze kujitokeza na kujisajili TaESA ili serikali iweze kubaini wananchi wenye ujuzi na sifa za kuweza kufanya kazi kwenye mradi huu wa bomba la mafuta na gesi", amesema Chandaruba.
Aidha, Mradi huo unatarajiwa kuchukua kati tya miezi 24 hadi 36 na unategemewa kuzalisha fursa za ajira takribani 10,000 wakati wa ujenzi na ajira zaidi ya 1,000 wakati wa uendeshaji wake.
"Ili kuhakikisha kwamba watanzania wengi wananufaika na fursa za ajira zitakazotokana na mradi huo, wakala unapenda kuwahamasisha watanzania wote wenye taaluma na ujuzi katika sekta ya mafuta na gesi kujisajili TaESA ili waweze kuingizwa kwenye kanzidata ya Wakala kwa lengo la kuiwezesha serikali kubaini idadi halisi ya watanzania walio na sifa zinazohitajika na walio tayari kuajiriwa kwenye mradi huo", amesisitiza Chandaruba.
Pamoja na hayo, Chandaruba ameendelea kwa kusema "nafasi hizi ni nafasi ambazo haziitaji gharama yeyote ile katika kujisajili au kutambuliwa".
Mradi wa Ujenzi wa Bomba la Kusafirisha Mafuta Ghafi “East Africa Crude Oil Pipeline (EACOP)” kutoka Hoima nchini Uganda hadi Chongoleani, Tanga nchini Tanzania unategemewa kuwa na urefu wa kilometa 1,445 ambapo ujenzi wa kilometa 1,115 za bomba hilo utafanyika nchini Tanzania. Jumla ya wilaya 24 na vijiji 184 hapa nchini vinategemewa kupitiwa na bomba hilo katika mikoa 8 ya Kagera, Geita, Shinyanga, Tabora, Singida, Dodoma, Manyara na Tanga.
No comments