Mshambuliaji kutoka nchini Uganda na klabu ya Simba ya Tanzania Emmanuel Okwi, amesema wanawaheshimu wapinzani wao katika mchezo wa marudiano wa kombe la Shirikisho Al Masry lakini hawawaogopi.
Simba itashuka dimbani kesho usiku kucheza na Masry wakiwa na kumbukumbu ya kulazimishwa sare ya mabao 2-2 katika uwanja wa Taifa na miamba hiyo.
Okwi ambaye tayari amefunga mabao matatu kwenye michuano hiyo amesema anafahamu mchezo utakuwa mgumu lakini wamejipanga kuhakikisha wanaibuka na ushindi.
Mganda huyo amesema wataingia uwanjani kesho kupambana ili kuipa Simba ushindi na kufuzu hatua inayofuata ingawa amekiri haitakuwa kazi rahisi.